Wednesday, April 2, 2014

Na Sweetbert Lukonge
HALI si shwari Yanga, wachezaji wa timu hiyo, kipa Juma Kaseja na beki wake, Kelvin Yondani wamekalia kuti kavu ndani ya klabu hiyo na huenda wakatimuliwa baada ya kutuhumiwa kuihujumu katika mechi yake ya Ligi Kuu Bara dhidi ya JKT Mgambo kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, wikiendi iliyopita.
Wachezaji hao wanadaiwa kupokea mamilioni ya fedha kutoka Azam ili wacheze chini ya kiwango.
Beki wa Yanga, Kelvin Yondani.
Katika mechi hiyo iliyokuwa na ushindani, Yanga ilitandikwa mabao 2-1 ambayo yanadaiwa yalitokana na uzembe uliofanywa na wachezaji hao na kuiweka timu hiyo kwenye mazingira magumu ya kutetea ubingwa wake.
Habari za uhakika ambazo Championi Jumatano limezipata kutoka ndani ya Yanga, zimedai kuwa hivi sasa uongozi wa timu hiyo unawafanyia uchunguzi Kaseja na Yondani ili kujiridhisha kama kweli walichukua mamilioni hayo ya Azam.
Imedaiwa kuwa endapo itabaini kuwa ni kweli walipokea mamilioni hayo ili wacheze chini ya kiwango na kuifungisha timu hiyo katika mechi hiyo, basi watachukuliwa hatua kali za kinidhamu ambazo hazijawahi kutokea katika klabu hiyo tangu kuanzishwa kwake.
“Kaseja na Yondani ndiyo watuhumiwa wakuu wa tuhuma hizo na wanachukiwa vibaya sana hivi sasa na viongozi kwani hata baada ya mechi walikuwa na wakati mgumu, walisemwa sana huku wakituhumiwa kupokea hongo kutoka Azam ili wacheze chini ya kiwango.
“Hata hivyo uongozi hivi sasa upo katika uchunguzi kabambe juu ya jambo hilo na endapo itabainika kuwa ni kweli walichukua fedha kutoka Azam, watachukuliwa hatua kali za kinidhamu kama viongozi wanavyodai lakini siwezi jua ni adhabu gani,” alisema mtoa habari huyo ambaye yupo ndani ya klabu hiyo.  
Alisema jambo ambao linawauma zaidi viongozi wote wa klabu hiyo ni kupoteza mchezo huo dhidi ya JKT Mgambo ambao umewaweka katika mazingira magumu ya kutetea ubingwa wao wa ligi kuu kutokana na kuwa nyuma kwa tofauti ya pointi saba na wapinzani wao Azam ambao wanaongoza msimamo wa ligi hiyo.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu, hakuwa tayari kuzungumza lolote juu ya tuhuma hizo wanazopewa wachezaji hao na kumtupia mpira ofisa habari wake, Baraka Kizuguto ambaye alisema:
“Taarifa za Yanga zinatolewa na uongozi kama ulivyofanya wakati ukitoa adhabu kwa kiungo wa timu hiyoAthuman Idd ‘Chuji’, hivyo kama tuhuma hizo ni kweli basi uongozi utatoa taarifa na siyo mtu mwingine.”
Katika mchezo huo Kaseja alipiga mpira kizembe ambao alirudishiwa na Yondani na kunaswa na Fully Maganga ambaye alitupia bao la kwanza la timu yake wavuni.
Yondani analaumiwa kuwa alicheza rafu ya kizembe ambayo ilisababisha penalti iliyopigwa na Balimi Basungu.
Matokeo haya yameiweka Yanga kwenye hali ngumu ya kutwaa ubingwa msimu huu kwani kwa sasa ina pointi 46 zikiwa ni saba nyuma ya Azam iliyopo kileleni na pointi 53.
via GPL

0 comments:

Post a Comment