Tuesday, April 1, 2014

NABII Josephat Mwingira na mwanamke anayedaiwa kuzaa naye, Dk. Phils Morris Nyimbi wameburuzwa katika Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi mjini Moshi wakidaiwa kuchukua shamba la ubia kati ya Mzungu Profesa Wade Sapp na Kampuni ya  Global 2000 (2010) International.
Nabii Josephat Mwingira.
Kwa mujibu wa hati za mashitaka zilizopo katika mahakama hiyo (nakala yake tunayo), kampuni hiyo ipo Dallas/Fort Worth, Marekani na ina matawi yake nchini Peru, Ghana, Liberia, Sierra Leone, Kenya na Tanzania ambako imesajiliwa mwaka 2002.
Katika shauri hilo ambalo ni namba 24 la mwaka 2013, litatajwa  Aprili 8, mwaka huu  mjini Moshi mbele ya Jaji Ama-Isario Munisi, imedaiwa kuwa mlalamikiwa wa kwanza  Dk.
  Phils Morris Nyambi na mlalamikiwa wa pili, Nabii Josephat Mwingira ambaye ni kiongozi wa Kanisa la Efatha, wamechukua shamba la hekari 37  la kampuni hiyo lililopo Bomang’ombe, wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro bila ridhaa yao.
Profesa Wade Sapp (kulia) anayedaiwa kuwaburuza mahakamani, Nabii Mwingira na Dk. Phils Morris Nyimbi (kushoto).
Imedaiwa mahakamani hapo kuwa mzungu huyo, Profesa Wade Sapp ambaye ni mwanasayansi na mwekezaji kwa niaba ya kampuni hiyo alituma fedha ambazo ni dola za Kimarekani 30,000  Desemba 21, 2006 kwa mlalamikiwa wa kwanza na akalipa kwa mwenye shamba aitwaye Philimon Ngilisho Mushi shilingi 10,000,000 kama kianzio huku tukio hilo likirekodiwa kwenye video.
Hati ya mahakama iliyoandaliwa na Wakili Desidery Ndibalema  wa  Kampuni ya Bin Attorneys anayemuwakilisha mzungu na kampuni hiyo imesema kwamba Dk. Phils Machi 30, 2007 alilipa kiasi kilichobaki  cha shilingi 20,000,000  kwa mwenye shamba baada ya kupewa na mzungu huyo. 
Wakili Ndibalema  ameeleza kuwa Januari 14, 2009 Dk. Phills bila kuwa na idhini ya Profesa Sapp au kampuni yao, alimpatia shamba hilo mlalamikiwa Nabii Mwingira ambaye anadaiwa kuzaa naye mtoto, kama zawadi (Gift Deed) ambapo aliipa kazi Kampuni ya Geo Land Consult Ltd kupima eneo hilo.
Hata hivyo, mlalamikaji tayari ametuma maombi kwa kamishna wa ardhi wa Moshi ili eneo hilo lipimwe kwa nia ya kujenga hospitali, ofisi ya mazingira na hoteli ya nyota tano ili kuwa kumbukumbu ya Dk.
Betty Sapp (alifia Moshi kwa ajali miaka ya nyuma), ambaye alikuwa mke wa Profesa Sapp anayetarajia kuja kutoa ushahidi wa kesi hiyo.
Mlalamikaji ameiomba mahakama itangaze kuwa Kampuni ya Global 2000 (2010) International na  mzungu huyo kuwa ni wamiliki halali wa eneo hilo na kuwaamuru walalamikiwa kulipa gharama ya kesi hiyo na nyingine ambazo mahakama itaona inafaa.
Profesa Sapp alikuwa ni Rais wa Taasisi ya Wanasayansi ya Marekani na sasa amestaafu.
via GPL

0 comments:

Post a Comment