Tuesday, May 6, 2014

Mapato ya mechi ya kirafiki baina ya Taifa Stars na Malawi iliyochezwa juzi jijini hapa yamezua mzozo baada ya kuzuka kwa malumbano baina ya Chama cha Soka Mkoa wa Mbeya (Mrefa) waliotaka kupata mgawo, lakini walikataliwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ayoub Nyenzi, aliyesimamia mechi hiyo.
Katika mechi hiyo, zaidi ya Sh31.2 milioni zilipatikana na viongozi wa Mrefa walitaka kupata mgawo kama ilivyo desturi.
Hata hivyo, maombi yao yalikwama baada ya Nyenzi kuwakatalia.
Katibu wa Mrefa, Seleman Harubu alipoulizwa kuhusu mzozo huo, alimtaka mwandishi kuzungumza na mwenyekiti wa Mrefa, ambaye alipopigiwa simu naye alisema suala lolote la mechi hiyo litazungumzwa na Nyenzi.
Naye Nyenzi alipopigiwa simu alikiri kupatikana kwa Sh31.2 milioni katika mechi hiyo baada ya kuingia zaidi ya watu 6,000, na kwamba Mrefa hawakustahili mgawo katika mapato hayo.
Akifafanua, Nyenzi alisema hakukuwa na mzozo, bali viongozi wa Mrefa hawakuelewa taratibu za TFF kwamba mapato ya timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ ni ya TFF.
“Niliwaelewesha kwamba mapato yote ya mechi ya timu ya Taifa ni ya TFF na ndiyo yanayotumika kulipia ankara kwenye hoteli na mambo mengine,” alisema Nyenzi huku akisisitiza kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wamiliki wa uwanja ndiyo waliopata fedha hizo.
Hata hivyo, vyama vya mikoa hustahili kupata ,gawo kwenye mechi zinazohusisha klabu na si timu ya taifa.
 Katika mechi hiyo iliyofanyikja Jumapili, Stars ililazimishwa kwenda sare ya bila kufungana na Malawi ambayo ilichezesha wachezaji wengi vijana.

0 comments:

Post a Comment